Ebola:Wahudumu 400 wagoma Sierra Leone

Image caption Takriban watu 5,000 wamefariki Afrika Magharibi kutokana na Ebola

Zaidi ya wahudumu 400 wa afya wanaowatibu wagonjwa wa Ebola katika kliniki moja nchini Sierra Leone wamegoma.

Wahudumu hao wakiwemo wauguzi na wafanyakazi wengineo wanagoma kushinikiza kuwalipa dola miamoja kila wiki kwa kuhatarisha maisha yao kutokana na kuwashughulikia wagonjwa wa Ebola.

Kliniki hiyo iliyo mjini Bandajuma karibu na eneo la Bo, ni kliniki pekee ambayo wagonjwa wa Ebola wanatibiwa Kusini mwa Sierra Leone.

Kwingineko nchini Mali, muuguzi mmoja pamoja na mgonjwa aliyetibiwa na muuguzi huyo wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Idadi hiyo inafikisha watu watatu waliofariki kutokana na Ugonjwa huo nchini Mali.

Mgonjwa huyo ni mwanamume mganga wa kiisilamu aliyekuwa na umri wa miaka 50 na alikuwa ameingia nchini humo kutoka Guinea.

Alikuwa ametibiwa na muuguzi aliyefariki akiwa na umri wa miaka 25 mjini Bamako katika kliniki ya Pasteur ambayo kwa sasa imefungwa na kuwekwa karantini.

Vifo hivi havijahusishwa na kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka miwili aliyefariki kutokana na Ebola mwezi oKtoba.

Shirika la Afya Duniani limetangaza mlipuko huu wa Ebola kama janga la dunia.

Haki miliki ya picha AFP GETTY
Image caption Mtoto wa miaka miwili ndiy alikuwa wa kwanza kufariki kutokana na Ebola Mali

Kesi hii ya Mali imeibuka siku moja baada ya shirika la Afya Duniani kuwatoa watu ishirini na tano karantini waliodhaniwa kumkribia msichana wa miaka miwili aliyefariki Oktoba .

Walikuwa miongoni mwa watu 100 waliokuwa karantini.

Kisa cha mtoto huyo kuugua na kufariki kutokana na Ebola kimewashangaza sana maafisa wakuu kwani inaarifiwa alisafiri kwa basi kutoka Guinea kuja Mali.

Takriban watu 5,000 wamefariki kutokana na Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi hasa nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone.