Majaribio ya dawa ya Ebola A:Magharibi

Haki miliki ya picha
Image caption Majaribio haya yanatoa matumaini kwa wagonjwa wa Ebola Afrika Magharibi

Shirika la misaada ya matibabu la Medecins Sans Frontieres, limesema kuwa litafanya majaribio ya dawa mpya za kutibu ugonjwa hatari wa Ebola katika vituo vitatu kanda ya Afrika Magharibi.

Wafanyakazi wa shirika hilo, watatumia dawa aina mbili katika orodha ya madawa yaliyoidhinishwa na shirika la afya duniani pamoja na damu na chembechembe za majimaji ya damu yote yaliyokubaliwa na shirika hilo.

Lengo la majaribio hayo ni kuwaweka hai wagonjwa katika hatua ya kwanza muhimu ya majaribio hayo kwa siku kumi na nne za kwanza za mradi huo.

Taarifa hii inakuja huku idadi ya waliofariki kutokana na Ebola ikifika watu 5,160.

Mlipuko wa ugonjwa huo unaaminika kuwaathiri watu 14,000 wote wakiwa katika mataifa ya Afrika Magharibi.

Msemaji wa shirika la MSF, Annick Antierens,amesema kuwa shirika hilo linashirikiana na watafiti kutoka Uingereza, Ufaransa na Ubelgiji kuwapa wagonjwa matumaini ya kupona.

''Huu ni ushirikiano wa kimataifa ambao unatoa matumaini kwa wagonjwa kuweza kupata tiba ya kweli,'' alisema msemaji huyo.