Wapinga 'kuvuliwa' nguo Kenya

Image caption Maandamano hayo yamefanyika chini ya kauli mbiu 'My dress my choice'

Wanawake mjini Nairobi, Kenya leo wameandamana kupinga kitendo cha mwanamke mmoja kuvuliwa nguo wiki jana kwa madai kuwa alikuwa amevalia sketi fupi sana.

Wanawake wengi walikerwa na kitendo hicho wakisema kuwa kila mwanamke ana haki ya kuvalia mavazi yanayomfurahisha.

Hiyo wiki jana kanda ya video ilisambazwa kwa mitandao ya kijamii ikionyesha mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina hadi sasa akivuliwa nguo zake na wanaume katika kituo cha magari ya abiria kati kati mwa Nairobi.

Image caption Na wanaume walikuwepo kuwaunga mkono wanawake katika maandamano yao

Wanawake mashuhuri wakiwemo wasanii, wanasiasa na wanaharakati walilaani kitendo hicho wakihoji kwani mavazi ya mwanamke yanamhusu nini mwanamume ambaye sio mumewe wala jamaa yake.

Baadhi walikitaja kitendo hicho kuwa cha kinyama na kinachokiuka haki za wanawake.

Msanii mmoja mashuhuri Nyota Ndogo alinukuliwa akisema ikiwa wanaume wanawavua nguo wanawake kwa kile wanachosema ni mavazi yasiyo ya kiheshima, basi na wanaume wanaolegeza long'i zao na wao basi pia wavuliwe nguzo zao.