Bianchi kuendelea na matibabu Ufaransa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jules Bianchi dereva wa F1 wa timu ya Marussia aliyepata ajali katika mashindano ya Japanese Grand Prix Oktoba,5, 2014

Dereva wa magari ya langa langa ya Formula 1 Jules Bianchi ametoka katika hali ya kuwa mgonjwa mahututi na sasa anapua bila msaada wa mashine, wamesema wazazi wake katika taarifa yao.

Dereva huyo wa timu ya Marussia mwenye umri wa miaka 25, alijeruhiwa kichwani alipoligonga gari la kuvuta magari katika michuano ya Japanese Grand Prix Oktoba 5,2014.

Dereva huyo raia wa Ufaransa amehamishwa kutoka hospitali ya mjini Yokkaichi nchini Japan na kupelekwa katika hospitali ya Nice nchini Ufaransa kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo hali yake bado ni "mbaya" na bado hana fahamu.

"Karibu wiki saba baada ya Jules kupata ajali katika uwanja wa Suzuka, na kufuatiwa na kipindi chenye changamoto katika kurejesha mishipa ya fahamu, tunaweza kutangaza kuwa Jules amepiga hatua muhimu," wamesema wazazi wake Philippe na Christine Bianchi.

"Matibabu yake kwa sasa yanaingia katika hatua mpya kuhusiana na kuimarisha ubongo wake."

"Japokuwa hali yake imeendelea kuwa mbaya na huenda ikaendelea hivyo, iliamuliwa kuwa hali ya Jules iliimarika vya kutosha kumwezesha kuhamishiwa nchini kwake Ufaransa."

Wamesema walipata "ahueni" kuthibitisha kuwa mtoto wao amehamishiwa hospitali ya Le Centre Hospitalier Universitaire de Nice, "ambako aliwasili muda mfupi uliopita".

Haki miliki ya picha epa
Image caption Gari ya Formula 1 ya Jules Bianchi

Madereva wa Formula 1 walimkubuka Jules Bianchi kabla ya mashindano ya Russian Grand Prix wiki moja baada ya ajali hiyo.

Bianchi alipata majeraha ya kichwa wakati gari yake ilipoligonga trekta katika lililokuwa likivuta gari ya Adrian Sutil wa Sauber.

Timu ya Marussia ilikuwa na dereva mmoja wiki iliyofuata katika michuano ya Russian Grand Prix iliyofanyika Sochi, Urusi, ambapo mshindi wa mashindano hayo Lewis Hamilton alikabidhi ushindi wake kwa Bianchi.

Wazazi wake wamepongeza "huduma ya hali ya juu" aliyopatiwa mtoto wao Jules Bianchi katika hospitali kuu ya Mie General Medical Centre, Yokkaichi, wakisema "wana deni kubwa la shukrani kwa hospitali hiyo kutokana na huduma hiyo kwa mtoto wao".

Tangu kutokea ajali hiyo, chombo kinachosimamia mashindano ya Formula 1, FIA wameanza mpango wa kuweka mfumo katika magari hayo utakaohakikisha usalama, na utakaowalazimisha madereva kupunguza mwendo katika eneo la ajali.