Aliyewaua waume saba akamatwa Japan

Image caption Bi Kaheki aliambia wandishi wa habari kuwa hana budi ila kukabiliana na tuhuma za mauaji ya waume zake

Polisi nchini Japan, wamefanya msako katika nyumba ya mwanamke mmoja nchini humo ambaye alikamatwa kwa kushukiwa kumuua kwa kumpa sumu mumewe huku taarifa zaidi za vifo vya wapenzi wa zamani wa mwanamke huyo, zikiibuka katika vyombo vya habari.

Msako huo dhidi ya nyumba ya Bi Chisako Kakehi, umefanyika siku moja baada ya kuzuiliwa na polisi.

Uchunguzi wa kilichomuua mumewe Chisako aliyefariki Disemba 2013, wiki chache baada ya kufunga naye harusi uligundua kuwepo sumu aina ya Cyanide kwenye damu yake.

Polisi wanachunguza kifo cha aliyekuwa mume wa mwanamke huyo aliyeuawa mwaka 2012.

Kadhalika walitembelea nyumba ya mwanamke huyo, mjini Kyoto na Osaka siku ya Alhamisi, ambako walipata dawa zilizokuwa zimesagwa na kuchanganywa na biskuti ambazo alikuwa anatumia kuweka dawa hizo pamoja na vitabu kuhusu dawa za kulevya.

Vyombo vya habari vinasema kuwa Bi Kakehi alikutana na mumewe ambaye alikuwa na bima ya maisha kupitia huduma ya kuwakutanisha wapenzi. Alikuwa mumewe wa nne.

Kando na kifo cha mwanamume huyo, polisi pia wanachunguza kifo cha mchumba mwingine wa mwanamke huyo aliyezirai akiwa anaendesha pikipiki.

Wachunguzi walipata sumu aina ya Cyanide kwenye damu yake huku taarifa za awali zikisema kuwa kifo chake kilisababishwa na maradhi ya Moyo.

Waume watatu wa kwanza wa Bi Kaheki na wachumba wengine watatu, walikuwa kati ya umri wa miaka 54 na 75 walipofariki.

Vifo vyao vilitokea miaka michache baada ya kuoana au kuanza uhusiano wa kimapenzi naye.

Bi Kakehi, alianza uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine mwenye umri a miaka 75 ambaye alifariki baada ya kuugua punde baada ya kula na Kaheki katika mgahawa mmoja.

Polisi wanafanya uchunguzi wao wakishuku kuwa mwanamke huyo huenda alihusika na vifo vya wanaume hao wengine.