Shambulio laua tena Mombasa Kenya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Askari wa Kenya wakizingira Misikiti inayodaiwa kuwa na waumini wenye msimamo mkali wa kidini mjini Mombasa

Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya. Polisi walipambana na vijana walioingia katika Msikiti wa Swafaa eneo la Kisauni na mpaka sasa zaidi ya vijana 400 wanashikiliwa tangu kuanza kwa msako huo, mapema wiki hii.

Mwandishi wa BBC, Emmanuel Igunza anasema Msikiti huo ulifungwa jana baada ya polisi kuuvamia Jumatano, ambamo walipata magruneti, mabomu ya petroli na silaha nyingine. Hali ya wasi wasi bado imetanda katika mji huo wa pwani. Serikali imekwishafunga misikiti minne ambayo wanasema ina uhusiano wa watu wenye misimamo mikali ya imani ya kidini.

Haki miliki ya picha afp getty
Image caption Pamoja na kukamata silaha mbalimbali, polisi pia walikamata bendera nyeusi, alama ya kuunga mkono kundi la kigaidi la Al-Shabab la nchini Somalia

Awali polisi mjini Mombasa pwani ya Kenya walisema wamepata silaha nyingine zaidi yakiwemo mabomu katika msikiti wa tatu ambao ulifanyiwa upekuzi

Msako huo katika msikiti wa Swafaa mtaani Kisauni unakuja baada ya msako mwingine wa Jumatatu ambapo polisi pia walipata silaha ndani ya msikiti ambao wanasema hutumika kutoa mafunzo yenye itikadi kali.

Mtaa wa Kisauni ndiko vijana waliokuwa wamejihami kuwadunga visu watu wanne na kuwaua. Pia waliwashambulia kwa silaha nyingine.

Waziri wa usalama wa ndani, Joseph Ole Lenku anasema kuwa msako huo ulifanywa katika misikiti ambayo hutumiwa na watu wanaoeneza itikadi kali za kiisilamu kwa vijana ambao inadaiwa wanajiunga na kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Al Shabaab nchini Somalia.

Viongozi wa kiisilamu wamelaani misako hiyo katika Misikiti wakisema kuwa itachochea zaidi vijana kuendeleza itikadi kali za kidini.