Wanafunzi waandamana Malawi

Image caption Rais wa Malawi,Bingu wa Mutharika

Polisi nchini Malawi wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana kutounga mkono hatua ya Serikali kuwacheleweshea walimu mishahara.

Wanafunzi hao wenye umri wa kati ya miaka sita na 12, waliingia mtaani mjini Blantyre .

Takriban walimu 6,500 wa shule za Uma hawajalipwa tangu mwezi Mei, na takriban walimu 1,000 wamegoma kuingia darasani.

Nchi wahisani walisitisha msaada wa takriban dola milioni 150 baada ya Serikali ya Malawi kukumbwa na kashfa ya rushwa.

Wakaguzi wa hesabu walibaini mwaka jana upotevu wa dola milioni 60 fedha za Serikali.

Takriban kiasi cha asilimia 40 ya bajeti ya nchi hiyo hutolewa na nchi wahisani.

Vyombo vya habari vya Malawi vinasema Wizara za Serikali zinajiendesha kwa bajeti ya kiasi cha robo ya pesa wanayopatiwa kwa mwezi.

Wanafunzi walisikika wakiimba kuwa hawatasoma mpaka walimu wao walipwe ili waweze kurudi darasani.

Msemaji wa Wizara ya elimu Manfred Ndovi amethibitisha kuwa walimu hao hawakulipwa tangu mwezi Mei na waliweza kurekodi walimu 2,800 pekee katika orodha ya malipo mwezi Septemba.

Amesema mchakato huu umekuwa changamoto kwa sababu unahusisha hazina, ofisi ya rasilimali watu na Wiazara yake.