Mtoto wa miaka 3 abakwa Afghanistan

Image caption Mtoto Neelofar alibakwa na mtu ambaye anajulikana kwa familia yake

Kwa kimya kingi, mtoto Neelofar mwenye umri wa miaka mitatu pekee amepakatwa na nyanyake katika kiti cha nyuma cha texi ikimkimbiza hospitalini.

Ndani ya mwili wake kuna kijipaipu ambacho amewekewa kutumiwa kumpa dawa kama huduma ya kwanza kabla ya kufikishwa hospitalini.

Mkono wake mmoja umefungwa kwa bandeji ambako kuna kifaa kinachotumiwa kuingizia maji mwilini mwake.

Mtoto Neelofar yuko hali mahututi, baada ya kubakwa na anahitaji matibabu maalum ambayo anaweza kupokea tu hospitalini.

Siku chache zilizopita, Neelofar alikuwa anacheza na rafiki zake nje ya nyumba yao wakati mwanamume mmoja alimteka na kwenda naye katika shamba lililokuwa karibu na nyumba hiyo.

Kulingana na familia yake na wahudumu wa afya, mbakaji alimfunga kinywa mtoto huyo na kumbaka na hata kujaribu kumuua.

Kwa karibu mtoto huyo ana majeraha mabaya na pia anahisi uchungu mwingi wakati akiendelea kupokea matibabu hospitalini.

Mwanamume huyo alimziba pua na mdomo mtoto kujaribu kumkosesha pumzi mtoto kwa sababu aliogopa kwamba angepiga mayowe. Mtoto huyo alikuwa ana alama nyingi shingoni mwake dalili ya majereha aliyoyapata.

Wazazi wa mtoto huyo hawakuwa nyumbani wakati wa kitendo hicho cha unyama.

Kwa bahati nzuri, familia ya mtoto inasema kuwa mwanamume aliyekuwa anapita karibu na nyumba hiyo ndiye alisikia mayowe yake na kumuokoa.

Neelofar alipatikana akivuja damu na akiwa ametupwa karibu na msikiti katika kijiji hicho.

Polisi wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 18 kuhusiana na unyama huo.

Inaarifiwa kuwa mwanamume huyo ni jirani na mtu anayejulikana kwa familia ya mtoto huyo.