Farc wagoma kumuachia Jenerali Colombia

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ruben Dario Alzate, Jenerali wa kwanza kutekwa nyara nchini Colombia

Waasi wa nchini Colombia, Farc wamesema wataahirisha zoezi la kuachiwa kwa kiongozi wa juu wa jeshi, na watu wengine wanaoshikiliwa mateka, kwa sababu ya uwepo wa wanajeshi wa serikali katika eneo wanaposhikiliwa mateka hao.

Katika taarifa ya waasi, wamedai kuwa kumekuwa na wanajeshi wengine katika jimbo la Choco.

Serikali iliahirisha kufanyika kwa mazungumzo ya amani yaliyokuwa yakifanyika kati yake na waasi nchini Cuba baada ya kutekwa nyara kwa Jenerali Alzate.

Waasi walisema wanampango wa kuwaachia mateka siku ya jumanne.

Jenerali Alzate alitekwa nyara pamoja na Wanajeshi wawili tarehe 16 mwezi huu.

Siku ya Jumamosi, Rais wa Colombia Juan Manuel Santos alitangaza kuwa Waasi wa Farc wameridhia kuwaachia mateka hao wiki hii bila kutaja tarehe.

Lakini hivi sasa waasi wamesema hawawezi kufanya kama walivyoahidi kutokana na yanayoendelea sasa.

Ruben Dario Alzate ni jenerali wa kwanza nchini Colombia kutekwa katika mgogoro uliodumu kwa kipindi cha miaka 50.

Timu ya wawakilishi wa Farc kwenye mazungumzo ya amani imesema kuwa wanajeshi wamefika katika eneo wanaposhikiliwa mateka hali inayosababisha kuahirishwa kwa zoezi hilo mpaka pale hali itakapokuwa shwari.

Inakisiwa kuwa watu 220,000 wamepoteza maisha tangu ulipotokea mzozo nchini Colombia.