Halle Berry amshitaki aliyekuwa mumewe

Image caption Muigizaji Halle Berry pia anasema kuwa aliyekuwa mumewe Gabriel alikuwa akitolea matamshi ya kibaguzi ya rangi

Muigizaji maarufu wa Marekani Halle Berry, ameghadhabishwa mno na hatua ya aliyekuwa mumewe juu ya kumbadilisha mwanawe rangi ya ngozi pamoja na kuweka kemikali kwenye nywele zake ili ziwe singa.

Muigizaji huyo alikasirishwa na jambo hilo kwani mwanawe mwenye umri wa miaka sita Nahla Berry ambaye kawaida anakuwa na nywele koto ameanza kubadilika.

Hapo ndipo hasira zilimpanda Halle Beryy kiasi cha kumpeleka mahakamani babake mtoto huyo Gabriel Aubry waliyeachana naye mwaka 2010.

Berry alinukuliwa akisema,'' kila siku wasiwasi unanizidi kuhusu athari atakazopata mwanangu Nahla kisaikolojia na kimwili kwa kuwekewa kemikali kwa nywele. Pia ataathirika kimawazo kutokana na mwili wake kuanza kubadilishwa.''

Pamoja na taarifa yake Berry aliweka picha za mwanawe za kabla na sasa ili kuonyesha jinsi mwanawe alivyobadilishwa rangi yake ya mwili huku nywele zake zikiwekwa kemikali ili kuwa singa.

Image caption Berry na aliyekuwa mumewe Gabriel Aubry

''Nataka mahakama kumuamuri babake mtoto huyu Gabriel kukoma juhudi zake za kubadilisha mwonekano wa mtoto wetu na labda kumsababisha mtoto kuanza kujiuliza kwa nini rangi nyeusi ya ngozi yake sio nzuri au haifai.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Jumatatu na wakili wa Berry ambaye hakufika mahakamani. Inaarifiwa jaji jaji aliamuru kwamba kuanzia sasa, babake Nahla lazima akome kumbadilisha mwonekeno wa mtoto.

Halle Berry na Aubry waliachana mwaka 2010 na jaji aliamua kuwa wote wawili hawana ruhusa ya kubadilisha sura na mwonekano wa mtoto wao kivyovyote.

Kwa mujibu wa jarida la TMZ, Halle Berry anahofia kuwa Aubry anajaribu kumfanya mwanawe kuwa mweupe na kwamba hataki afanane kama Mmarekani mweusi.

Hapo awali, Berry mwenyewe alisema kuwa mwanawe ni marekani mweusi kama yeye mwenyewe. Babake mtoto buyo ana asili mchanganyiko ya Canada na Ufaransa .