Ebola:Rais Hollande kuzuru Guinea

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Hollande ni rais wa kwanza kuzuru kanda ya Afrika Magharibi ambako mlipuko wa Ebola unahangaisha mamilioni

Rais wa Ufaransa Francois Hollande anatarajiwa kuwasili nchini Guinea , na kuwa Rais wa Kwanza kutoka Ulaya kutembelea nchi hiyo iliyoshuhudia mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa wa Ebola katika kanda ya Afrika Magharibi.

Rais Hollande atatoa ujumbe wa umoja katika vita dhidi ya Ebola kwa watu wa Guinea ambako zaidi ya watu 1,200 wamefariki kutokana na Ebola.

Ufaransa imeahidi kutoa mchango wa dola milioni 125 ili kusaidia katika jitihada za kupambana na ugonjwa huo kwa kufungua vituo kadhaa vya matibabu ya ugonjwa huo.

Shirika la afya duniani WHO, lilisema kuwa mlipuko huo umekuwa janga katika kanda ya Afrika Magharibi

Image caption Chanjo mpya ya Ebola inafanyiwa majaribio na wanasayansi wanasema chanjo hiyo inaonyesha matumaini

Bado kuna visa vipya vimeripotiwa katika maeneo ya Kusini Mashariki lakini hali inaimarika katika sehemu nyinginezo.

Zaidi ya watu 5,400, wameathirika kutokana na ugonjwa huo huku mataifa ya Guinea, Sierra Leone na Liberia yakiathiriwa zaidi kuliko nchi nyinginezo.

Rais Hollande anatarajiwa kuwasili nchini Guinea Baadaye leo ,na kuwa rais wa kwanza kutoka Ulaya kutembelea Guinea tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Ebola kuripotiwa mwezi Machi.

Wakati wa ziara yake ya siku moja, Hollande atazuru vituo vya afya na kuhudhuria vikao vya majadiliano kuhusu janga la Ebola, kulingana na shirika habari la AFP.

Pamoja na hilo, Ufaransa inapanga kutuma vituo vya afya vya kuhamahama pamoja na kununua vitanda 200 vitakavayotumiwa na wagonjwa wa Ebola.