Hasira baada ya Mubarak kufutiwa makosa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji Misri

Polisi nchini Misri wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji wanaopinga hatua ya mahakama nchini humo kutupilia mbali kesi ya mauaji dhidi ya Rais aliyeondolewa madarakani Hosni Mubarak.

Zaidi ya watu 2000 walikusanyika katika viunga vya Tahrir mahala ambapo ndipo zilipozaliwa harakati za mapinduzi ya nchi hiyo mwaka 2011.

Awali Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha jela ambapo kwa sasa anatumikia pia kifungo cha miaka mitatu kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kwa sasa Hosni Mubarack anashikiliwa katika hospitali ya jeshi ambako pia anapatiwa matibabu.

Waziri wake wa zamani wa mamabo ya ndani Habib al-Adly na wenzake sita walihukumiwa kifungo cha maisha 2012, inakadiriwa takriban watu 800 waliuawa wakati wa harakati za kumuondoa kiongozi huyo Februari 11.2011.