Waandamanaji wavamia ofisi za serikali Hong Kong

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Polisi wakabiliana na waandamajani waliovamia ofisi za serikali Hong Kong

Wanaharakati wanaopigania demokrasia katika eneo la Hong Kong, wamesababisha ofisi za serikali kufungwa asubuhi ya leo kufuatia usiku wenye ghasia kwenye mitaa.

Maofisa 11 wa polisi walijeruhiwa na watu 40 kukamatwa huku kampeni hiyo ikiingia mwezi wa tatu.

Serikali ya mji wa Hong Kong ililaani ghasia hizo ikisema kuwa waandamanaji waliwarushia vifaa polisi.

Waandamanaji hao ambao wengi ni wanafunzi wanataka China kuipa Hong Kong uhuru zaidi wa kumchagua kiongozi wao kwenye uchaguzi unaokuja.

Kadhalika waandamanaji hao, walikabiliana na polisi waliokuwa wamejihami kwa virungu na malori ya maji wakiwarushia watu maji.

Jumatatu asubuhi amri ilitolewa ya kutimuliwa kwa waandamanaji hao kutoka katika eneo walilokuwa wanafanyia maandamano yao.

Maandamano ya leo yamesababisha hofu ya ghasia au vurugu zaidi kutokea miezi miwili tu baada ya maandamano mengine kutokea miezi miwili iliyopita.

Waandamanaji hao wanasema wanataka wao kama watu wa Hong Kong kuruhusiwa kuchagua viongozi wao katika uchaguzi wa mwaka 2017 bila ya serikali ya China kuingilia kati.

China hata hivyo imesema itaruhusu wakazi wa Hong Kong kuchagua viongozi wao lakini itawakagua wagombea wa nafasi ya waziri mkuu kabla ya uchaguzi kufanyika.

Baada ya makabiliano ya Jumatatu asubuhi, kiongozi wa eneo hilo, aliwaonya waandamanaji hao kutorejea katika eneo la maandamano