Boko Haram wavamia miji 2 Nigeria

Image caption Nia kuu ya Boko Haram ni kuwa na dola ya kiisilamu inayofuata sheria za kiisilamu

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram wamefanya mashambulizi katika miji miwili eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

La kwanza lilikuwa la kujitoa mhanga pamoja na shambulizi lengine katika kituo cha polisi cha Damaturu.

Wenyeji wa mji wa Maiduguri walielezea kusikia milipuko miwili kwenye soko moja.

Mashambulizi mengine ya kujitoa mhanga eneo hilo wiki iliyopita yaliwaua zaidi ya watu 70.

Mapema leo Jumatatu watu wanaokisiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram waliteketeza kituo cha polisi katika mji wa Damataru kilicho umbali wa kilomita 100 Magharibi mwa mji wa Maiduguri.

Inaarifiwa watu 5 wameuawa katika mashambulizi hayo ya mabomu yaliyotokea katika soko lililokuwa na watu wengi.

Mjini Damaturu , milipuko na milio ya risasi ilisikika huku wanamgambo hao walipokuwa wanashambulia mjini huo.

Boko Haram imeahidi kubuni dola ya kiisilamu katika maeneo ambayo kundi hilo linadhibiti.

Milipuko hio ilitokea Jumatatu katika soko la Maiduguri , mji mkuu wa jimbo la Borno ambayo ilisababishwa na wasichana wawili waliojilipua.

Takriban watu 32 walijeruhiwa katika milipuko hio.