Mnada wa ripoti kuhusu Biko wasitishwa

Image caption Familia ya Biko inapinga kuuzwa kwa ripoti kuhusu kifo cha marehemu

Mahakama nchini Afrika Kusini imesitisha, mnada wa ripoti kuhusu kifo cha mwanaharakati maarufu aliyepigania vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, Steve Biko.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa familia ya marehemu Biko.

Familia yake imesema kuwa ripoti hiyo ni sehemu ya nyaraka za historia ya nchi hio na kwamba haipaswi kuuzwa kwa manufaa ya watu binafsi.

Dalali mmoja alikuwa amepanga kuuza ripoti hio iliyotolewa kutoka kwa mmoja wa maafisa wa uchunguzi wa kifo ya Biko.

Biko alifariki mikononi mwa polisi mwaka 1997. Kifo chake kilizua ghadhabu kubwa katika jamii ya kimataifa.

Mahakama pia ilizuia kuuzwa kwa ripoti kuhusu mauaji ya mpigania uhuru mwingine Ahmed Timol, aliyefariki pia akiwa chini ya uangalizi wa polisi mwaka 1971.

Wote wawili walikuwa na umri wa miaka 29 walipofariki.

Mwanawe Biko ndiye alitoa taarifa ya kusema kuwa madalali waliokuwa na nia ya kuuza ripoti hiyo wamezuiwa na mahakama kufanya hivyo.

Nyaraka kuhusu kilichomuua Biko zilikua zinahifadhiwa na familia yake na inaarifiwa kuwa mamake ndiye alizikabidhi kwa mmoja wa wachunguzi aliyeteuliwa kuhudhuria vikao vilivyokuwa vinajadili kilichosababisha kifo cha Biko.

Familia ya Biko pamoja na Timol zinailamu iliyokuwa serikali ya kibaguzi kwa vifo vya wawili hao, wakisema kuwa waliteswa kabla ya kuuawa wakiwa kizuizini.

Hata hivyo utawala huo ulikanusha madai hayo.