Hali bado tete mjini Mandera

Image caption Hali ya usalama bado ni tete mjini Mandera Kaskazini Mashariki mwa Kenya

Hali ya taharuki imetanda mjini Mandera mpakani mwa Kenya na Somalia baada ya mashambulizi mapya yaliyotokea Jumanne na kusababisha mauaji ya watu 36 wengi wao wakiwa sio waislamu.

Hatua hiyo imemfanya Rais wa Nchi hiyo Uhuru Kenyatta kumuachisha kazi waziri wa usalama wa ndani na mkuu wa polisi.

Inaarifiwa kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa serikali wanaoishi katika eneo hilo wameanza kulihama kwa hofu ya usalama wao.

Wakati huohuo, msemaji wa Rais Uhuru Kenyatta ameonya kuwa kushinda vita dhidi ya wapiganaji wa Al Shabaab huenda ikachukua muda mrefu sana.

Bwana Manoah Esipisu aliyasema hayo baada ya wapiganaji hao kuwaua watu 36 waliokuwa kwenye machimbo ya kokoto mjini Mandera karibu na mpaka na Somalia.

Esipisu, aliambaia BBC kwamba, serikali inafanya kila iwezalo kuzuia mashambulizi lakini haiwezi kuahidi kwamba hapatatokea shambulizi lengine.

Alisema wanajeshi wa Kenya wataendelea na operesheni yao nchini Somalia dhidi ya Al Shabaab hadi wakenya watakapohakikishiwa usalama wao.