Aishi na maiti akitarajia itafufuka

Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Maiti

Familia moja nchini Canada iliishi na maiti katika chumba cha juu cha nyumba yao kwa miezi sita kwa kuwa waliamini marehemu atafufuka iwapo wataendelea kumuomba mungu,lakini mwili huo ukapatikana baada ya familia hiyo kushindwa kulipa mkopo waliochukua kununua nyumba hiyo.

Kaling Wald mwenye umri wa miaka 50 alipatikana na makosa ya kushindwa kuwaarifu maafisa wa polisi kwamba mumewe alifariki ,kosa ambalo na akahukumiwa kuwekwa katika muda wa majaribio na ushauri,wakili wake alikiambia chombo cha habari cha Reuter siku ya Jumanne.

Peter Wald mwenye umri wa miaka 52 alifariki mnamo mwezi machi mwaka 2013 kwa kile mamlaka inasema ni sababu za kawaida kufuatia maambukizi ya mguu wake yanayodaiwa kusababishwa na ugonjwa wa sukari.

Mkewe Kaling Wald alimwacha kitandani na kufunga chumba hicho katika nyumba yao ya Hamilton ,Ontario ili kuzuia harufu kali iliokuwa ikitoka chumbani humo kuwafikia watu waliokuwa wakiishi nyumbani humo.

Kama vile Yesu alivyomfufua Lazaro baada ya siku ya nne ,pia yeye aliamini kwamba Mungu atamfufua mumewe wakili wa mwanamke huyo alisema.