Serikali yakana tishio la njaa Sudan.K

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Marial Benjamin

Waziri wa mashauri ya Nchi za kigeni wa Sudan Kusini Barnabas Marial Benjamin, amepuuzilia mbali tahadhari iliotolewa kua taifa hilo changa limo katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.

Afisa mmoja mkuu wa umoja wa mataifa ambaye ndio mwanzo amefika Sudan Kusini kufanya kazi kama naibu mshirikishi mkuu wa utoaji msaada wa dharura, Kyung-wha Kang, amesema kuwa watu milioni mbili unusu wamo katika hatari ya kuangamizwa na baa la njaa kwa sababu ya ukosefu wa chakula.

Amesema hiyo ni kutokana na mapigano mapya na hali tete ya usalama nchini humo.

Image caption Watu wakipokea msaada wa chakula Sudan Kusini

Lakini waziri wa nchi za kigeni wa Nchi hiyo, Barnabas Marial Benjamin, ameiambia BBC kuwa mavuno yalikuwa bora na hofu ya kutokea kwa baa la njaa haliko.

Aidha ameongeza kusema kuwa kuna matumaini ya muafaka wa amani kati ya Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar, ambaye kufikia sasa hajakubali kuhudumu kama waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa.