Watoto wauawa kikatili DRC

Wanajeshi wa DRC wakielekea kwenda kupigana na ADF Haki miliki ya picha AFP

Inaarifiwa kuwa watu kama 30 waliuwawa katika mashambulio kwenye vijiji mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Taarifa zinasema kuwa mashambulio hayo yalifanywa Jumamosi usiku kwenye vijiji karibu na mji wa Beni ambako watu zaidi ya 250 wameuawa tangu mwezi Oktoba.

Wakuu na mashirika ya raia yanawalaumu wapiganaji kutoka Uganda wa kundi la ADF, lakini baadhi ya wadadisi wanasema hakuna ushahidi wa kutosha wa kuhusisha kundi hilo.

Mwandishi mmoja wa habari katika eneo hilo aliambia BBC kuwa waliofariki ni pamoja na wanawake na watoto ambao walibururwa kutoka kwa nyumba zao na kukatwa katwa kwa mapanga.

Alisema haijulikani nani aliyefanmya mashambulizi hayo, ingawa maafisa wakuu wamelaumu kundi la waasi la Uganda la ADF.

Alisema maelfu ya watu wameachwa bila makao kutokana na vurugu zinazoendelea na kwamba wanahofia sana kurejea makwao.