UN yaomba mabilioni ya dola

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Umoja wa mataifa umezindua ombi kubwa zaidi la pesa kuwahi kutolewa katika historia yake la dola bilioni 16 ili kufadhili mipango yake ya kibinadamu kote duniani.

Ombi lengina kubwa kuwahi kutolewa na Umoja huo ni la Syria ambapo liliomba dola bilioni saba kuwasaidia wale walioathirika na vita vya Syria.

Ombi hilo linajiri wakati mashirika ya misaada yanaonya kuwa yameishiwa na fedha za kukimu oparesheni za mwaka huu.

Wiki iliyopita, shirika la mpango wa chakula duniani lilitangaza kuwa limelazimika kupunguza msaada wa chakula kwa wakimbizi wa Syria.

Mwaka mmoja uliopita, Umoja wa mataifa uliomba dola bilioni 13 za Marekani, kwa utoaji misaada duniani - nchini Syria, Sudan Kusini, au Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Lakini hiyo ilikuwa kabla ya mgogoro uliojiri Ukraine, kabla ya kuzuka kwa kundi la Islamic State Iraq, na kabla ya janga la Ebola. Dola bilioni 13 hazikutosha - na pesa hizo hazikutolewa kikamilifu na nchi wafadhili.

Na sasa unapojaribu kukabiliana na mahitaji ya mwaka huu, mashirika ya misaada ya umoja huo, yataomba fedha za miezi 12 ijayo. Chakula na vifaa vya matibabu kwa wakimbizi vinafaa kununuliwa mapema, hospitali zinahitajika na zinafaa kujengwa.

Misaada ya kibinadamu haipatikani mara moja, mashirika ya misaada yanahitaji kupanga, lakini ili kufanya hivyo, yanahitaji fedha.

Ombi la mwaka 2015 litadhihirisha mizozo mingi iliopo duniani na changamoto kubwa zinazoyakabili mashirika ya umoja huo yakijaribu kuwasaidia wale waliokumbwa na migogoro hiyo.