Museveni ataka Afrika kujiondoa ICC

Image caption Rais Museveni alialikwa kwa sherehe za kuadhimisha miaka 51 ya uhuru wa Kenya zilizofanyika mjini Nairobi

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kwa mara nyingine amekeji mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu ICC akisema inakandamiza bara la Afrika.

Kauli ya Museveni imekuja baada ya kiongozi wa mashataka wa mahakama hiyo Fatou Bensouda kumwondolea mashtaka Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha miaka 51 tangu Kenya ijipatie Uhuru mjini Nairobi Museveni amesema kuwa atapeleka mswada katika mkutano wa Umoja Afrika wa kuzitaka nchi zote za bara Afrika kujiondoa katika uanachama wa ICC.

Kadhalika ameshutumu Mahakama hiyo na kusema kuwa inapendelea kuwadhulumu viongozi wa kiafrika.

Naibu Rais wa Kenya ambaye anakabiliwa na kesi katika mahakama hiyo William Ruto amesema kuwa ana hakika kesi yake itatupiliwa mbali jinsi ilivyofanyika katika ile Uhuru Kenyatta akitaja kesi hiyo kuwa iliathiriwa na siasa.

Rais Museveni alikua kwenye sherehe hizo kwa mwaliko wa serikali ya Kenya. Viongozi wengine walioalikwa kweny sherehe hizo ni Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Ghana John Mahama.