Mtoto amuibia nyanyake na kuwashangaza wengi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wazazi wa Alexis wanasema wana afueni mtoto wao yuko salama

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11 aliiba maelfu ya dola kutoka kwa nyanyake na kisha kukodi taxi kumpeleka eneo la mbali kukutana na kijana mwenye umri wa miaka 16 ambaye walikuwa wakiongea naye tu kupitia mtandao wa Internet.

Wawili hao hawajawahi kuonana hata siku moja.

Msichana huyo Alexis Waller yuko salama na bukheri wa afya na hatakabiliwa na kesi yoyote baada ya kitendo chake ambacho kimewashangaza wengi.

Maafisa wanasema Waller aliiba dola elfu kumi kutoka kwa chumba cha nyanyake katika mji wa Bryant, jimbo la Arkansas.

Baada ya kitendo chake cha wizi, msichana huyo alikodisha taxi na kumtaka dereva kumpeleka kwa kijana huyo katika jimbo la Florida.

"nilisema nitaka kwenda mjini Jacksonville, Florida," Waller aliambia shirika la habari la KARK. "kijana huyo aliniuliza kama nina pesa na nikamwambia ndio. ''

Gharama ya safari yake ilikuwa dola 1,300.

Jarida la Arkansas Democrat-Gazette linasema kuwa Waller alikuwa tayari amesafiri umbali wa maili 500 kuelekea kwa kijana huyo lakini polisi waliweza kuwasiliana na dereva wa taxi hio na kuwafuata.

Wazazi wake walisema Waller aliwakasirisha sana lakini ni afunei kwao kwani mtoto wao aliweza kurejea nyumbani.