Nigeria kwafukuta mgomo viwandani

Image caption Kiwanda cha mafuta kikifuruma uzalishaji

Nchini Nigeria muungano wa vyama viwili vikuu vya wafanyakazi kwenye sekta ya mafuta wametoa tamko la kuanza kwa mgomo mkubwa wa kitaifa nchini humo. Vyama hivyo kwa kifupi PENGASSAN na NUPENG wameorodhesha mlolongo wa madai ikiwa ni pamoja na migogoro ya kazi na hali mbaya ya usafishaji mafuta nchini humo.

Maafisa wakuu kutoka muungano huo wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya mafuta wameiambia BBC mgomo huo wan chi nzima ndio kwanza umeanza na hautakwisha mpaka hapo serikali ya nchi hiyo watakapo shughulikia madai yao.

Ikiwa mgomo huo utaendelea kwa Zaidi ya siku mbili raia watalazimika kupanga foleni kubwa watakapotaka kuuziwa bidhaa hiyo muhimu, kwani uhaba hautaepukika.

Si mara ya kwanza hilo kutokea- Na kila hali hiyo ikijiri bei za mafuta hupanda na wengine kulazimika kupata bidhaa hiyo kwa kwa bei ya juu zaidi katika soko lisilo rasmi.

Vyama hivyo vya wafanyikazi PENGASSAN na NUPENG vimwahi kutishia kufanya mgomo nchini humo mara kadhaa na wadadisi wanasema wana uwezo wa kuikwamisha serikali endapo migomo yao itafaulu.

Awali viongozi wa vyama hivyo walikuwa wakishinikiza kurejeshewa kazini maafisa wakilishi wa wafanyikazi waliokuwa wamefutwa kazi na makampuni ya mafuta.

Lakini sasa orodha ya madai yao imeongezeka na sasa inajumuisha matakwa ya bei za mafuta kupunguzwa , kusitishwa kwa vitendo vya wizi wa mafuta, ucheleweshwaji wa kupitishwa kwa mswada wa kuboreshwa kwa secta ya mafuta na hata kuboreshwa kwa miundo mbinu kama barabara na kadhalika.

Zaidi ya hayo wanalalamika kuwa serikali hiyo ya Nigeria imeshindwa kufanyia ukarabati viwanda vya usafishaji mafuta nchini humo.

Viwanda vya kusafisha mafuta vimetelekezwa kwa miaka mingi nchini humo hivyo kulazimu nchi hiyo iliyona utajiri mkubwa wa mafuta kuishia kuagiza mafuta yaliyosafishwa kutoka nje kwa matumizi ya kitaifa,biashara ambayo inaendeshwa na mtandao wa baadhi ya matajiri wakubwa nchini humo huku ikgubikwa na rushwa nzito nzito.

Ni bayana mengi ya Madai ya muungano huo huenda yasitekelezeke kwa haraka hasa wakati huu nchi hiyo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu .Kwa mfano ni ndoto kudhania viwanda vya usafishaji mafuta vinaweza kufanyiwa ukarabati katika kipindi cha mda mfupi.

Huenda vyama hivyo vya wafanyikazi vijaribu kulazimisha serikali iwalipe kiinua mgongo cha cha kutuliza mgomo huo hivyo wajipatie hela ya matumizi ya msimu huu wa sikuukuu ikiwo zawadi za kusherehekea Christimas.