Watatu wauawa tukio la utekaji Sydney

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tony Abbot waziri mkuu wa Australia

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amesema mtu mwenye bunduki aliyehusika na utekaji nyara watu katika mkahawa mmoja jijini Sydney alikuwa akijulikana kwa vyombo vya serikali na alikuwa na historia ndefu ya uhalifu, akiwa amegubikwa na itikadi kali za kidini na kuwa na hitilafu ya akili.

Watu wawili waliuawa, pamoja na Mwislam aliyejihami kwa bunduki baada ya makomandoo kuvamia mkahawa huo uliopo eneo la kibishara jijini Sydeney, na kumaliza tukio la utekaji nyara lililodumu kwa saa kumi na sita.Watu wanne walijeruhiwa katika tukio hilo, ikiwa ni pamoja na askari polisi aliyepigwa na vipande vya risasi.

Mtu huyo mwenye silaha alitambuliwa kuwa mkimbizi kutoka Iran, aliwashiklia mateka watu kadha katika mkahawa wa Lindt.

Image caption Mwaathirika wa tukio la utekaji nyara Sydney, Australia

Mtu huyo aliyejihami kwa silaha alijulikana kwa jina la Man Haron Monis. Alipata hifadhi ya kisiasa nchini Australia mwaka 1996 na alikuwa nje kwa dhamana akikabiliwa na mashitaka kadha.

Eneo la katikati ya jiji la Sydney lilifungwa wakati mtu mwenye silaha alipowashikilia mateka watu mapema Jumatatu, akiwalazimisha baadhi yao kunyanyua juu dirishani bango jeusi la Kiislam katika mkahawa wa Lindt.

Mkahawa wa Lindt Chocolat Cafe uko katika mtaa wa Martin Place, eneo lenye pilika pilika nyingi za kibiashara mjini Sydney.

Waziri Mkuu Tony Abbott amesema "tukio la kutisha" katika mkahawa kulikuwa na "hali ya kutisha kuzidi maelezo" na kulikuwa na "kitu cha kujifunza" kutoka tukio hili la kigaidi".

"matukio haya yanaonyesha kuwa hata kwa nchi yenye uhuru, yenye uwazi na ukarimu kama nchi yetu, bado inakabiliwa na vitendo vya ghasia zenye msukumo wa kisiasa lakini pia yanaonyesha kuwa tuko tayari kukabiliana nayo," aliwaambia waandishi wa habari.

Image caption Eneo ulipo mkahawa Lindt katikati ya jiji la Sydney, Australia

Bendera zitapepea nusu mlingoti katika eneo lote la New South Wales kuwaenzi waathirika wa tukio hilo la utekaji nyara.

Mwanaume mwenye umri wa miaka 34 na mwanamke mwenye umri wa miaka 38 walithibitika kufa baada ya kupelekwa hospitali, kama ilivyokuwa kwa mtu mwenye silaha limesema jeshi la polisi katika taarifa yake kutoka eneo la New South Wales

Wanawake wawili walipata majeraha yasiyotishia uhai kama ilivyokuwa kwa polisi ambaye alipigwa usoni na vipande vya risasi.

Mwanamke mwingine alipata majeraha kwa kupigwa risasi katika bega lake.