Mashirika yasio ya kiserikali yafutiwa leseni kenya

Haki miliki ya picha .
Image caption Mswada mpya wa usalama unasemekana kukiuka haki ya watu kujieleza

Serikali ya Kenya imefutulia mbali leseni za mashirika 510 yasio ya kiserikali ikiwemo 15 ambayo yametuhumiwa kuhusika na ugaidi.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa afisa mmoja mkuu wa serikali ambaye amesema kuwa serikali pia imepiga tanji akaunti za benki za mashirika hayo pamoja na kufutilia mbali vibali vya kazi vya wafanyakazi wa kigeni wa mashirika hayo.

Kenya imechukua hatua hii kufuatia mjadala mkali nchini humo kuhusiana na mswada tatanishi unaolenga kupambana na ugaidi.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Kenya likilalamikia hatua ya serikali kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia.

''Mashirika hayo yamefutiliwa leseni zao mbali kwa sababu ya kukosa kupeana rekodi zao za kifedha'', alisema Henry Ochido, naibu mkuu wa bodi ya ushirikiano ambayo inasimamia mashirika hayo.

Bwana Ochido alisema kua mashirika 15 miongoni mwa yale yaliofungwa yanashukiwa kufadhili harakati za kigaidi.

Uamuzi wa kufutilia mbali leseni za mashirika hayo, bila shaka utazua gumzo katika nchi ambayo wengi wanahofia serikali inatumia tisho linlaotokana na kundi la al-Shabab kukandamiza uhuru wa watu kujieleza.

Wiki jana bunge la Kenya lilipitisha mswada ambao umezipa taasisi za usalama na mashirika ya ujasusi mamlaka makubwa kuhusiana na maswala ya kuhakikisha usalama wa nchi.