Ebola:Msako wa wagonjwa kufanywa S.Leone

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma ametaka kufanyika kwa msako wa nyumba hadi nyumba kwa waathiriwa wa ugonjwa wa ebola nchini humo.

Rais Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone amesema kuwa msako wa nyumba kwa nyumba unaanza kote nchini humo kuwatambua watu walio na ugonjwa hatari wa ebola.

Aidha, Rais huyo amepiga marufuku biashara siku ya Jumapili.

Katika hotuba kupitia televisheni ya taifa, Koroma amesema kwamba usafiri kutoka wilaya moja hadi nyingine ni marufuku.

Ebola

Takwimu kufikia Disemba 14

6,900

Jumla ya watu waliokufa

  • 3,290 Liberia

  • 2,085 Sierra leone

  • 1,525 Guinea

  • Mali :8

Juma moja lililopita, wakuu walifutilia mbali mikutano yote na sherehe za siku kuu ya krismasi na mwaka mpya kama njia ya kukabiliana na kusambaa zaidi kwa ebola.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde kutoka shirika la afya Duniani WHO, Sierra Leone ni taifa ambalo limeathirika pakubwa na ebola ambapo zaidi ya visa elfu nane vimeripotiwa.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maafisa wa kukabiliana na Ebola wakitembea katika mitaa ya Sierra Leone.

''Musiwafiche wagonjwa'',alisema rais.

Mbali na kufutilia mbali biashara za siku ya jumapili,mikakati hiyo mipya itashirikisha mda wa kununua bidhaa siku ya jumamosi na katikati ya wiki.

Mji wa Freetown umerekodi zaidi ya asilimia 50 ya maambukizi ya ugonjwa wa ebola nchini Sierra leone katika kipindi cha majuma mawili yaliopita.

Mwandishi wa BBC nchini Sierra Leone Umaru Fafana amesema kuwa mikakati hiyo inalenga kudhibiti makundi ya watu.

Amesema kuwa wakaazi wa mji wa Freetown wanaendelea kujumuika katika barabara mbali na kufanya mazoezi kwa pamoja licha ya tishio hilo la Ebola.