Dhahabu nyeupe kuinufaisha Tanzania

Haki miliki ya picha AP
Image caption Shamba la pamba

Ingawa Tanzania ina eneo kubwa zaidi ya nchi zote za Afrika linaloweza kutumika kulima zao la Pamba bado imeachwa mbali katika suala la uzalishaji na nchi nyingine ikiwamo Mali, Burkanafaso, Afrika Kusini, Sudan na Misri.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Gabriel Mwalo amesema iwapo mipango mipya waliyojiwekea itafanikiwa Pamba ya Tanzania itarejesha hadhi yake ya kuitwa Dhahabu nyeupe na kuweza kutumika katika uimarishaji uchumi wa mkulima na nchi kwa ujumla.

“Hatufanyi vizuri kwa kuwa wakulima hatujajipanga ili kuzalisha kiasi kikubwa katika hekari. Lakini pia wenzetu wameendelea wanatumia kilimo cha umwagiliaji wakati sisi kilimo chetu asilimia mia moja tunategemea mvua” Gabriel Mwalo amesema hayo akijibu kwa nini Tanzania imezidiwa na nchi ambazo zina maeneo madogo yanayofaa kwa kilimo.

Swali la kujiuliza ni kwa nini bei ya Pamba haionekani kumlipa mkulima,badala yake inamdidimiza? kaimu mkurugezi amesema gharama za uzalishaji ni kubwa lakini kiasi cha Pamba anachopata mkulima ni kidogo wakati anayeamua bei ya Pamba ni Soko la dunia.

“Hapa kilicho cha muhimu ni kuzalisha zaidi katika eneo dogo yaani kuzalisha kwa tija. mkulima anapaswa kuhakikisha anapata kiwango kikubwa cha Pamba katika eneo hilo alilonalo ili hata bei ikishuka bado apate fedha nzuri”

Ili kupambana na tatizo la uchafuzi wa Pamba unaofanywa kwa lengo la kuongeza uzito kwa udanganyifu ikiwamo kuchanganya mchanga na maji ndani ya Pamba, Mwalo amesema suluhisho ni kuwaondoa mawakala na badala yake kihimizwe kilimo cha Mkataba kati ya mnunuzi na mkulima na washirikiane tangu mwanzo wa kupanda hadi pamba inapokuwa tayari kununuliwa.

Sekta ya Pamba ikisimamiwa vizuri inaweza kuliletea taifa kipato cha fedha za kigeni kufikia zaidi ya dola milioni 100 za Marekani kwa mwaka na pia kuinua maisha ya watu takribani milioni 15 iwapo lengo la kuzalisha marobota laki 7 ya pamba kwa mwaka litafikiwa ifikapo mwaka 2020.