Serikali ya Uganda kuridhiana na Sejusa

Image caption David Sejusa.serikali ya Uganda imesema kuwa inataka kuridhiana naye ili arudi katika wadhfa wake.

Serikali ya Uganda imesema kuwa itaanzisha mazungumzo ya maridhiano na Jenerali David Sejusa,kwa jina lingine Tinyefuza, ili kumrai arejee kwenye wadhfa wake.

Generali Sejusa alitoroka nchi hiyo mwezi Aprili mwaka 2013 alipodai,kupitia barua aliyoiandika kuwa kulikuwa na njama ya kuwaondoa maafisa wa ngazi za juu serikalini waliopinga ''mradi wa Muhoozi''

Bregedia Muhozi Kainerubaga,kamanda wa kikosi maalum cha jeshi,ni mwanawe Rais Museveni.

Kulingana na gazeti la The Monitor nchini Uganda,Waziri Mkuu Ruhakana Rugunda,wakati wa kikao cha kila wiki cha maswali na majibu bungeni,aliwaambia wabunge kuwa serikali itafanya kila iwezalo ili kuleta upatanishi kati yake na Jenerali Sejusa, kama vile imekuwa ikifanya na wale isiyokubaliana nao siku zilizopita.

Alikuwa akijibu swali alilouliza mbunge wa Manispaa ya Mukono,Bi Betty Nambooze,aliyetaka kujua serikali itachukua hatua gani dhidi ya Jenerali Sejusa ambaye ''alitoroka jeshi na kwenda uhamishoni''.

''Majumba ya habari yalifungwa na Jenerali Sejusa alipoteza kiti chake bungeni.

Maafisa wa serikali walitaja uhalifu dhidi yake.Je,serikali inapanga kumshtaki katika mahakama ya kijeshi?Bi Nambooze aliuliza na kusababisha msisimko bungeni.

''Nina imani mheshimiwa Nambooze amefurahi kama vile wengi wetu kuwa Jenerali Sejusa amerejea.

Image caption Waziri mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda

Serikali itamtendea kama vile imekuwa ikiwatendea watu wengine kama yeye ambayo ni kutupatanisha na kuhakikisha kuwa ametulia kwa amani nchini,''alijibu Daktari Rugunda.

''Kisa chake kinafaa kuwa ishara kwa yeyote anayeishi uhamishoni kwa kuhofia usalama wake kuwa Uganda ni nchi yetu na wanakaribishwa kurejea nyumbani wakati wowote.''aliongezea.

Jenerali Sejusa,katika mahojiano yake ya kwanza na wanahabari tangu kurejea kutoka uhamisho wa kujitakia wikendi iliyopita,alisema kuwa amerejea nchini kupiga vita tabia ya kutoheshimu sheria na mapambano kurejesha kuheshimu sheria.

''Niliondoka mwezi Aprili tarehe 31 chini ya usafiri wa kawaida.

Nilifika nchini Uingereza siku iliyofuatia na kujua kwamba wasaidizi walikuwa wamekamatwa na kwamba nilikuwa nikamatwe pia.

Nilienda na kukata tikiti ya kuabiri ndege ya Uingereza kurudi tarehe 9 mwezi Mei mwaka 2013 lakini serikali iliwatuma wanajeshi katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

Kwa hivyo,nikafikiri halikuwa jambo bora mimi kurejea,''Jenerali Sejusa alisema.