Marufuku kutoa wafanyakazi wa nyumbani UG

Image caption Bendera ya Uganda

Bunge nchini Uganda limepitisha azimio ambalo linazuia usafirishwaji wa mabinti na wanawake kwenda kufanya kazi nje ya nchi hiyo na azimio hili limekuja baada ya kushuhudia vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa jinsia hiyo kutoka kwa waajiri wao.

Marufuku hiyo inafuatia waziri wa watu wazima na wale wenye ulemavu , Sulaiman Madada,ameeleza kuwa serikali ya Uganda inatambua juu ya unyanyasaji huo na imepokea malalamiko ya waathirika wa vitendo hivyo hasa Uarabuni kwa waganda wanaofanya huko.

Hata hivyo ,ameongeza kuwa suala la ajira ni muhimu mno wakati huu ili kuwapatia Waganda ajira,wakati huohuo serikali ya Uganda ikiongeza nafasi za ajira kwa wajariramali wadogo na mpaka sasa makampuni ishirini na manne yalipewa leseni ya kupeleka wafanyakazi nje.

Kufuatia hali hiyo,wabunge wameilaumu Serikali ya Uganda kwa kushindwa kuwasaidia Waganda waliokata tamaa huko ughaibuni na kuwaacha katika dhiki kuu wakiwa katika makampuni hayo waliyowapa leseni ambayo yanaangalia faida wapatayo na sio majaaliwa ya waganda hao.

Malalamiko mengi ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono yamewafikia wanaharakati wa haki za binadamu na kudai kwamba waganda wanalia kuingiliwa kwa nguvu kinyume na maumbile na waajiri wao

Naye mbunge Medard Sseggona ameeleza kuwa Waganda wengi wanataotafuta ajira nchi za kigeni wanasaini mikataba wakiwa wamekata tamaa na kesi zao huwezi kuzipeleka mahakamani.

Wabunge wawili Elijah Okupa na Sabiti waliibua hisia za watu nchini humo baada ya kutoa ushuhuda wa binti mmoja ambaye ametupwa jela na mwajiri wake mjini Kuwait ,ambaye ametoa wito kwa wabunge na serikali kuingilia kati suala lake .

Msichan huyo kwa muujibu wa Okupa,anadai kuwa amegeuka kuwa mtumwa wa ngono kwa mwajiri wake.

Azimio kama hilo lilikuwa mwaka 2009,dhidi ya kampuni ya Uganda Veterans Ltd ambayo ilikuwa ikipeleka mabinti kutoka Uganda kwenda kufanya kazi Iraq ama Marekani ambao waliishia kuteswa na familia za wa Iraq ambao walikuwa wakikabiliana na manyanyaso makubwa bila mshahara.

Wasichana hao mara wanapofika Ughaibuni hunyang’anywa pasi za kusafiria ,na huamriwa kufanya kazi kinyume na makubaliano ya awali.Takwimu zinaonesha kuwa waganda wpatao 42,015 waliondoka nchini humo kuelekea Mashariki ya kati kwenda kutafuta ajira tangu mwaka 2006 na hawajaonekana tena nchini mwao.