Rais wa Ufaransa awatuliza raia wake

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Ufaransa

Rais wa Ufaransa amewataka raia wake wasishtushwe na visa vya kushambuliwa kwa polisi na raia katika kipindi cha siku kadhaa.

Rais Francois Hollande ameyasema hayo baada ya mtu mmoja kuendesha gari na kulivurumisha katika soko la Krismasi lililosheheni watu, magharibi mwa mji wa Nantes na kujeruhi watu kumi.

Waendesha mashtaka wamesema, shambulizi hilo linafanana na lile lililotokea katika mji wa Dijon siku ya Jumapili ambapo dereva wa gari aliyekuwa akisema kwa sauti maneno ya kiislamu mfululizo alipowagonga wapita kwa miguu katikati mwa mji.

Na siku ya Jumamosi, mtu mmoja alipigwa risasi na kufariki baada ya kumchoma kisu afisa wa polisi karibu na mji wa Tours.

Hata hivyo, wachunguzi wamesema matukio hayo hayana uhusiano na waislamu wenye msimamo mkali, lakini mwandishi wa BBC amesema hofu imetanda nchini Ufaransa kuhusiana na idadi ya watu wanaojiunga na makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve, amesema tishio lipo nchini humo na kuwahakikishia wafaransa kwamba kila kitu kinafanywa ili kuhakikisha usalama wa raia wake.