Wahisani bado wanashikilia misaada TZ

Image caption Mwenyikiti wa wahisani ambaye ni balozi wa Finland nchini Tanzania ,Sinikka Antila.

Mjadala mkali umeingia siku ya pili nchini Tanzania kufuatia Rais wa nchi hiyo Jakaya Kikwete kulihutubia taifa la nchi hiyo ambaye pamoja na mambo mengine alitangaza kumfuta kazi waziri mmoja kwa kuhusika na kashfa ya uchotaji wa mamilioni ya fedha kwenye akaunti ya Escrow.

Upande wa upinzani umekosoa hotuba hiyo na kusema Rais Kikwete alipaswa kutangaza kuwafuta kazi mawaziri na watendaji wengine waliotajwa kwenye azimio la bunge lilipelekwa kwake hivi karibuni.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete alitangaza kumfuta kazi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka katika hotuba yake hapo jana ambaye ni mmoja ya mawaziri wanaodaiwa kuhusika na kashfa ya ufisadi ya kuhamisha isivyo halali fedha kwenya akaunti ya Tegeta Escrow.Hotuba hiyo Rais Kikwete tangu jana imezua mjadala mkali nchini Tanzania ambao wengi wamekuwa na maoni tofauti.

Chama Kikuu cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimekosoa hotuba hiyo na kusema kimesikitishwa na hatua alizozitangaza Rais Kikwete hapo jana.Hivi karibuni Bunge la Tanzania lilipitisha maazimio manane ambapo miongoni mwa maazimio hayo ilikuwa ni pamoja na serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu wanaodaiwa kuhusika katika sakata hilo.

Miongoni wa watendaji hao ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania TANESCO pamoja na maafisa na watendaji wengine wanaodaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo.

Hata hivyo katika hotuba hiyo Rais Kikwete mbali ya kumfuta kazi waziri huyo mmoja, hakusema kama Waziri wa Nishati na Madini atachukuliwa hatua za kinidhamu lini zaidi ya kusema anamweka kiporo waziri huyo huku akisubiri uchunguzi dhidi ya waziri huyo jambo linalopingwa na upande wa upinzani.

SAHIHISHO

Wakati hayo yakiendelea kundi la wahisani wa kimataifa ambao walisitisha misaada ya takribani dola milioni 500 kwenye bajeti ya Tanzania wamesema kupitia kwa Mwenyikiti wao ambaye ni Balozi wa Finland nchini Tanzania, Sinikka Antila, kuwa wamepokea maelezo aliyotoa Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi alivyokubali kutekeleza maazimio ya Bunge.

Katika mawasiliano yake kwa njia ya barua pepe, alisema hakuna fedha ambazo zimetolewa na wahisani hao baada ya hotuba ya Rais Kikwete, bali ni jumla ya fedha zilizotolewa kufikia sasa ambazo ni asilimia 15 ya kiasi kilichoahidiwa.

Kwa upande mwingine upande wa chama kinachotawala CCM kupitia kwa Katibu Mwenezi wa vijana wa chama hicho Paul Makonda amesema wanaipongeza hotuba ya Rais Kikwete na hatua alizochukua.

Hotuba hiyo ya Rais Kikwete huenda itaendelea kuleta mjadala Tanzania kwa siku kadhaa kufuatia uzito wa kashfa hiyo ambayo imeitikisa taifa hilo.