Sahihisho:Wahisani bado wanaikaba Tanzania

Image caption Balozi wa Finland nchini Tanzania, Sinikka Antila.

Tunachukua fursa hii kurekebisha taarifa tuliyoitoa jana katika tovuti yetu yenye kichwa cha habari "Wahisani wafurahishwa na hotuba ya JK".

Kimsingi, katika mawasiliano yake na Idhaa ya Kiswahili ya BBC kwa njia ya barua pepe, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Sinikka Antila, ambaye pia ni mwenyekiti wa Wahisani wanaochangia bajeti ya Tanzania (Budget Support Development Partners) alieleza kuwa wamekuwa wakifuatilia hatua zinazochukuliwa kuhusiana na madai ya "uchotwaji" wa fedha kutoka akauti ya Tegeta Escrow.

"Wahisani walipokea hatua ya kuwasilishwa ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) Bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuwasilishwa kwa ripoti ya PAC Bungeni, mjadala uliofuatia, maazimio yaliyopitishwa na Bunge", Balozi Anitila aliifahamisha BBC.

Washirika wa maendeleo (DPs) wanaamini kuwa mifumo ya uwajibikaji ya Tanzania itamudu kushughulikia swala hili kikamilifu na tunatazamia kupatikana kwa majibu ya uhakika kutoka serikalini.Balozi Antila alifafanua kuwa wamefuatilia maelezo aliyoyatoa Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa.

"Wahisani wamepokea taarifa aliyoitoa Rais tarehe 22 Disemba, 2014, akitambua maazimio yaliyopitishwa na Bunge na kuthibitisha baadhi ya hatua na uchunguzi zaidi. Wakati bado tunatathimini hali ya mambo, wahisani bado wanaendelea na mashauriano na Wizara ya Fedha, na uamuzi wowote wa kuruhusu fedha zitolewe utafanyika kwa mawasiliano na Waziri anayehusikaā€¯, alieleza Balozi Antila.

Pia alisema mpaka sasa, kiasi cha dola za kimarekani milioni 84, au takriban asilimia 15 ya fedha zilizoahidiwa kusaidia bajeti (Budget Support funds) kwa mwaka 2014/15 zilikwishatolewa, lakini fedha hizo hazina uhusiano na hatua zinazochukuliwa sasa. Bali ni jumla ya fedha ambazo zimetolewa kwa nyati tofauti.

Tunaomba radhi kwa Balozi Sinikka Antila wa Finland na pia wasomaji wa tovuti ya bbcswahili.com kwa usumbufu uliojitokeza .