Kiongozi wa Al-Shabaab akamatwa

Image caption Kundi la wapiganaji wa Al shabaab

Maafisa nchini Somali wanasema kuwa kiongozi mkuu wa kundi la wapiganaji wa Alshabaab amekamatwa karibu na mji mmoja karibu na mpaka wa Kenya na Somali.

Kamishna wa Wilaya ya El Wak mjini Gedo ameiambia BBC Somalia kwamba vikosi vya usalama vilimkamata Zakariya Ismail Ahmed Hersi katika maficho yake ndani ya nyumba moja baada ya kupashwa habari.

Mwaka 2012 Marekani ilitoa zawadi ya dola millioni 3 kwa yeyote yule ambaye angeweza kutoa habari za Hersi.

Kundi la Al Shabaab limejiondoa kutoka miji kadhaa nchini Somalia tangu uzinduzi wa mashambulizi makali dhidi ya kundi hilo yanayotekelezwa na vikosi vya AMISOM vikishirikiana na wanajeshi wa serikali ya Somalia.

Bwana Hersi alikuwa kiongozi wa kundi la Alshabaab upande wa Amniyat.

Mapema mwaka huu alikosana na kiongozi wa kundi hilo Ahmed Abdi Godane ambaye aliuawa katika mashambulizi ya Marekani mnamo mwezi Septemba.