Wafanyakazi wa kikristo waachiwa Libya

Haki miliki ya picha na
Image caption Mji wa Sirte unaoshambuliwa na wapiganaji wenye silaha.

Wafanyakazi kumi na watatu Wakristo kutoka Misri wameachiliwa huru baada ya kukamatwa nchini Libya.

Siku ya Jumamosi watu walioshuhudia tukio hilo katika mji wa kaskazini wa Sirte wamesema watu wenye silaha waliwachukua wanaume hao wa Kikristo kutoka eneo la makazi usiku wa manane.

Lakini mtawala wa kikabila alisisitiza Jumatatu kuwa walizuiliwa na watu wenye kufanya biashara haramu ya watu sio kwamba walitekwa.

Tukio hili ni karibuni zaidi katika mfululizo wa matukio ya hivi karibuni kuwasibu Wakristo wa Misri wanaofanyakazi nchini Libya.

Wakazi wa eneo hilo wanasema watu hao wenye silaha waliokuwa wameficha sura zao waliwatenganisha Wakristo na Waislam kabla ya kuwafunga pingu na kuondoka nao katika magari.

Muftah Marzuq, mkuu wa baraza la wazee katika mji wa pwani wa Sirte, amesema watu hao waliachiliwa baada ya mazungumzo kati ya watu wenye silaha na maafisa wa mji huo.

"Wamisri walikamatwa na kikundi cha watu kinachojishughulisha na biashara haram ya watu, kwa sababu ya mgogoro unaohusisha fedha na usafirishaji kwenda jimbo la Harawa mashariki mwa Sirte," Bwana Marzuq amewaambia waandishi wa habari.

Habari za kupotea kwao ziliibuka wakati chanzo cha habari kilicho karibu na serikali kilipokishutumu kikundi cha Kiislam cha Ansar al-Sharia kwa kuwateka Wakristo 13.

Tukio hili limekuja siku chache baada ya Wakristo saba kutoka Misri kuripotiwa kutekwa katika kituo bandia cha ukaguzi katika mji wa Sirte walipokuwa wakijaribu kuondoka kutoka mji huo.

Libya ni makazi kwa jamii kubwa za waumini wa dini zote mbili za Waislam na Wakristo kutoka Misri, wengi wakifanyakazi katika sekta ya ujenzi.

Libya imejikuta katika machafuko na kukosa utulivu na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kung'olewa madarakani na kuuawa kwa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Wanamgambo wanaopingana kwa sasa wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi ikiwemo miji mikubwa miwili ya Tripoli na Benghazi, na mji wa Sirte yamekuwa makao salama kwa wapiganaji wa Kiislam.