UN yakemea mashambulizi dhidi ya Albino

Image caption Jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi wako hatarini kupoteza maisha

Umoja wa Mataifa umekemea wimbi la mashambulizi dhidi ya Watu wenye ulemavu wa ngozi, Albino, baada ya tukio la kutekwa kwa mtoto wa miaka minne mjini Mwanza, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Mwakilishi wa UN nchini humo Alvaro Rodriguez ameitaka Serikali ya Tanzania kuzidisha juhudi za kupambana na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya albino.

Akiwa katika ziara kanda ya ziwa, Mjumbe huyo wa UN amekemea kutekwa kwa binti mdogo na kutoa wito kwa serikali kufanya kila iwezalo kumuokoa na kumkutanisha na Familia yake.

Mtoto Pendo Emmanuel alitekwa akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Ndami baada ya Watu kadhaa wakiwa na mapanga kuvamia makazi yao tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.Polisi wamesema Watu 15 akiwemo Baba yake wamekamatwa wakihusishwa na tukio la kutekwa kwa mtoto huyo.