Teknolojia yaleta ahueni kwa walemavu

Image caption Idd akitumia Kompyuta

Kukua kwa sayansi na teknolojia duniani kunaleta matuini makubwa kwa walemavu wa macho. Uvumbuzi wa program mbaliombali umewafanya wale wasioona waweze kuiona dunia kwa namna yao.

Mmoja ya walemavu wa macho ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idd Said Mshindo kwa sasa anaweza kufuatialia mambo yote kupitia computer na mitando ya kijamii kwa kutumia Teknolojia ya Talk Back yaani program inayotoa sauti.

Mwandishi wetu wa Dar es Salaam Arnold Kayanda amekutana na mlemavu huyo ambaye anaweza kuitumia simu, Komputa na hata kuwasiliana kwenye ukurasa wake wa facebook kwa msaada wa teknolojia ya Talk Back katika simu, Talking Watch katika saa na Screen Reader katika computer.

Image caption Idd anaweza kutumia simu yake kama anayeona

Idd anasema watu wengi wakiona anavyobadilishana nao mawazo katika mitandao ya kijamii, hawaamini kama hawezi kuona chochote.

“Hata nilivyoanza kutumia simu ya mkononi watu hawakuamini nilivyokuwa napokea na kuwatumia ujumbe mfupi wa simu. Lakini zaidi wanashangaa ninavyowajibu katika ukurasa wa facebook hasa tunapojadili masuala ya mchezo wa soka. Wanaandika ninajibu papo kwa papo” Anasema Idd

Kijana huyu ambaye anamalizia masomo yake ya shahada ya kwanza ya ualimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam anasema kabla ya kuja kwa teknolojia ya Talk Balk alikuwa analazimika kuwa na rafiki ambaye atamsomea ujumbe wowote wa simu unaoingia.

“Kwa mlemavu wa macho hakuna ujumbe wa siri kwa kuwa ni lazima rafiki akusomee. Lakini nikiona anayeniandikia anaaandika meseji za utata yaana za mahusiano basi naweza kuandika jina ambalo rafiki yangu hatajua huyo aliyeniandikia ni nani” Anaeleza huku akiangua kicheko.