Utalii:TZ yailaumu Kenya kuhusu marufuku

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Uwanja wa ndege

Serikali ya Tanzania inatarajiwa kuingilia kati kuhusiana na marafuku iliowekewa magari ya Utalii ya taifa hilo yanayosafirisha watalii kati ya Arusha na Nairobi kutoingia katika uwanja wa Ndege wa JKIA jijini Nairobi.

Wahudumu wa magari hayo waligoma kwa masaa kadhaa wakingojea msimamo wa serikali kuhusu marufuku hiyo iliowekewa magari hayo ya tanzania mnamo mwezi Disemba mwaka jana.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, Waziri wa mali asli na utalii Lazoro Nyalandu amewahakikishia wahudumu hao kwamba atasafiri hadi jijini nairobi pamoja na wawakilishi wao ili kuzungumza kuhusu swala hilo na mwenzake wa Kenya.

''Serikali yetu pia imeshangazwa na hatua hiyo ya Kenya kwa sababu viwanja vya ndege havihusiki katika makubaliano yalioafikiwa na mataifa hayo jirani'',alisema.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Mbuga ya wanayama pori

Bwana Nyalandu amekiri kwamba Tanzania mwaka 1985 iliafikiana na kenya kupiga marufuku magari ya kenya ya Utalii kutoingia katika mbunga zake za wanayama pori,hatua ambayo ililenga kuwawezesha wahudumu wa magari ya Utalii ya nchini humo.

''Marufuku hiyo ya Kenya inamaanisha uwanja huo wa ndege sasa ni kivutio cha watalii badala ya eneo la kuingilia Kenya'',alishangaa Nyalandu akisema hatua hiyo imewagharimu wahudumu wa utalii nchini Tanzania.

Lakini wachanganuzi wanaamini kwamba marufuku hiyo ya Kenya ni hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya tanzania kufunga mpaka wa Bolongoja uliopo kati ya mbuga ya wanayama pori ya Serengeti na masai Mara ya Kenya miaka ya 70.