Seleka wadai malipo kwa kumkamata Ongwen

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waasi wa Seleka

Waasi wa kundi la Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanasema kuwa wanapaswa kutuzwa kwa kumkamata kamanda mkuu wa kundi la waasi la Uganda, LRA.

Kamanda huyo anasakwa na viongozi wa mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Dominic Ongwen, kamanda mkuu wa LRA alikabidhiwa wanajeshi wa Marekani wiki jana.

Marekani ilikuwa imeahidi kutoa kitita cha dola miliono 5 kama zawadi kwa atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa kamanda huyo, kuhamishwa kwake na hatimaye kufunguliwa mashitaka.

Kamanda mmoja mkuu wa Selekea alisema Ongwen alikamatwa baada ya makabiliano ya dakika 25 ambapo baadaye waliwaarifu wanjeshi wa Marekani wlaiokuwa katika eneo hilo.

Image caption Dominic Ongwen alikuwa naibu kamanda wa kundi la waasi wa LRA nchini Uganda

Hata hivyo afisaa mmoja wa Marekani alisema kwamba bwana Ongwen alijisalimisha kabla ya kukabidhiwa kwa vikosi vyao.

Waasi wa Seleka wenyewe walisababisha ghasia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa miezi kadhaa wakatiw alipouteka mji mkuu Bangui mwaka 2013.

Maafisa wakuu nchini Uganda wanasema kwamba Ongwen atapelekwa nchini Uganda katika siku chache zijazo.

Anajaulikana kwa jina "White Ant", jina lake la msituni na yeye ndiye naibu kamanda wa kundi la LRA Joseph Kony ambaye pia anasakwa na mahakama ya kimataifa ya ICC.

Kundi la LRA liliwateka nyara maelfu ya watoto na kuwalazimisha kupigana huku wasichana wakifanywa watumwa wa ngono.