Kamanda wa LRA kufikishwa ICC

Image caption Muasi Ongwen

Kamanda wa kundi la waasi la LRA nchini Uganda ambaye alijisalimisha katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Dominic Ongwen atakabidhiwa kwa mahakama ya kimataifa ya ICC, yasema serikali ya Uganda.

Kamanda huyo ni miongoni mwa watu wa kundi la LRA wanaosakwa na viongozi wa mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Waasi wa Seleka walioko katik Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako Ongwen alikamatwa walisema kuwa muasi huyo alikamtwa ingawa wanajeshi wa Marekani wanasema kuwa alijisalimisha.

Msemaji wa jeshi la Uganda, ameambia shirika la habari la Reuters kwamba Ongwen atakabidhiwa ICC na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako alijisalimisha.

Ongwen alikabidhiwa wanajeshi wa Marekani wiki jana na bado anazuiliwa na wanajeshi hao.

Marekani ilikuwa imeahidi kutoa kitita cha dola miliono 5 kama zawadi kwa atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa kamanda huyo, kuhamishwa kwake na hatimaye kufunguliwa mashitaka.

Maafisa wakuu nchini Uganda wanasema kwamba Ongwen atapelekwa nchini Uganda katika siku chache zijazo.

Anajaulikana kwa jina "White Ant", jina lake la msituni na yeye ndiye naibu kamanda wa kundi la LRA Joseph Kony ambaye pia anasakwa na mahakama ya kimataifa ya ICC.

Kundi la LRA liliwateka nyara maelfu ya watoto na kuwalazimisha kupigana huku wasichana wakifanywa watumwa wa ngono.