Aliyezikwa na Kifaranga kaburi lafukuliwa

Nchini Tanzania, hivi karibuni kulitokea mkasa wa kushtusha kuhusu mwanamke mmoja aliyekufa na kuzikwa na kifaranga cha kuku tumboni kama ishara ya kufukuza mkosi kwenye ukoo wake. Sasa kaburi la mwanamke huyo limekutwa limefukuliwa. Tukio hilo linalodaiwa kutokea katika mkoa wa Shinyanga, kaskazini magharibi mwa Tanzania limewashtua wengi na kuzua maswali kutokana na kutoeleweka lengo au maana yake.

Baada ya mazishi ya mwanamke huyo kutawaliwa na imani za kishirikina, ikiwa ni pamoja na kupasua tumbo lake na kuchinja kifaranga alichozikwa nacho sasa kaburi lake inadaiwa limefukuliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Katika picha ambazo BBC imeziona, kaburi linaloaminika kuwa la Bertha Steven, linaonekana kufukuliwa upande mmoja huku sanda ikionekana kwa nje.

Ingawa kwa kawaida mfu huachwa apumzike baada ya kuzikwa, mwanamke huyo, ameendelea kuandamwa.

Hata polisi wamehusishwa kubaini wahusika wa vitimbi hivyo. Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha ameieleza BBC kuwa tayari wameanza kuchunguza ili kuwapata watuhumiwa wa swala hilo.

Mila na desturi za baadhi ya makabila mkoani Shinyanga zinakataza wanawake kwenda mazikoni, lakini mara ya kwanza tukio hili kutokea, wazee wa kimila au wananzengo walisusia maziko ya mwanamke huyo baada ya baadhi ya ndugu kufanya kilichoelezwa kuwa ni tambiko hadharani.

Wakati huu pia ni wanawake ndiyo waliotoa taarifa za kukuta kaburi la mwanamke mwenzao likiwa wazi.