Guinea kutokomeza Ebola kwa siku 60

Haki miliki ya picha
Image caption Mila na tamaduni za Watu zimesababisha Watu wengi kupoteza maisha kutokana na Ebola

Mipango ya mamlaka za afya nchini Guinea ni kuutokomeza ugonjwa wa Ebola kwa siku sitini. Mpango huu unategemea kuhamasishwa kwa Watu katika maeneo yote yaliyoathiriwa nchini Guinea kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Wataalam wa afya wanasema maambukizi mapya hutokana na mazishi ya watu waliokufa kwa Ebola mazishi ambayo hufanywa na ndugu wa marehemu wakidai kuwa wanadumisha mila na utamaduni.

Katika mradi huu Wazazi wanaowaficha wagonjwa na kusababisha ugonjwa kusambaa ndani ya familia zao wanaguswa pia kwenye hatua hizi mpya zinazotekelezwa na Ofisi inayoshughulikia mapambano dhidi ya Ebola.

Jamii ya kimataifa imekuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha Guinea inafanikiwa katika mipango ya kupunguza idadi ya vifo na maambukizi yatokanayo na Ebola, hata hivyo jamii ya kimataifa inatoa wito kwa nchi hiyo kuwa makini katika kampeni yao mpya ya kumaliza ugonjwa huo kabisa ndani ya siku sitini.

Ugonjwa wa Ebola umegharimu maisha ya Watu elfu moja na mia nane nchini Guinea tangu ulipoanza mwaka mmoja uliopita lakini swali linaloulizwa hivi sasa ni je Ugonjwa huu utamalizwa kabisa kwa kipindi cha Siku sitini?