Ethiopia yawafunga waingereza 2 kwa 'ugaidi'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri mkuu wa Ethiopia (kulia) Hailemariam Desalegn amekuwa akikosolewa na kuwa na sheria kali za kupambana na ugaidi

Raia wawili wa Uingereza na msomali mmoja wamefungwa jela nchini Ethiopia kwa kupanga njama ya kuunda dola ya kiisilamu.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa kituo cha redio kinachounga mkono serikali.

Taarifa hii imethibitishwa na ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza.

Wanaume hao watatu waliohukumiwa kifungo cha kati ya miaka minne na saba walidaiwa kuwa na uhusiano na kundi la wapiganaji wa kiisilamu.

Ethiopia ina sheria kali sana za kupambana na ugaidi.

Kwa mda mrefu imekuwa ikiendesha harakati dhidi ya kundi la wapiganaji wa kiisilamu wa Al shabaab nchini Somalia.

Nchi hio pia imekuwa ikikabiliwa na madai ya kuwafunga jela wakosoaji wa serikali wakiwemo wanablogu maarufu nchini humo ambao wanakabiliwa na tisho la kufungwa jela kwa madai ya kuhusika na ugaidi na wamekuwa wakizuiliwa tangu Aprili mwaka 2014.

Hata hivyo kiongozi wa nchi hio ametetea sana sheria kali za ugaidi ambazo nchi hio hutumia.

Kulingana na FBC, washukiwa wawili waingereza, Ali Adros Mohammad na Mohammad Sharif Ahmed walikuwa wanaishi mjini London wakati Mohammad Ahmed akiwa na mizizi yake Hargeisa eneo la Somaliland.

Watuhumiwa hao watatu inaarifiwa walikuwa na mawasiliano na wanachama wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu tangu mwezi Disemba mwaka 2012 na walisafiri kwenda mjini Adama, ambako walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Mahakama kuu mjini Addis Ababa, iliarifiwa kuwa Ali Adros aliingia nchini Ethiopia kutoka Kenya kwa mafunzo ya kijeshi na kwamba pia alikuwa na makubaliano na kundi la waasi la (OLF), kufanya mashambulizi nao.