Waziri awaomba radhi wanafunzi Kenya

Image caption Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaisery

Waziri wa usalama nchini Kenya Joseph Nkaissery amewaomba radhi wanafunzi wa shule ya msingi waliofyatuliwa gesi ya kutoa machozi wakati walipokuwa wakiandamana kupinga unyakuzi wa kipande cha ardhi ambacho kilikuwa uwanja wao wa kuchezea.

Bwana Nkaissery amempa mnyakuzi wa ardhi hio siku moja kuondoa sehemu ya ukuta iliobaki baada ya wanafunzi kuuangusha na kisha kuondoka katika eneo hilo.

Nkaisery ameongeza kwamba serikali itaweka uzio katika ardhi hio na kuiwacha kuwa uwanja wa kuchezea wa wanafunzi hao.

Wakati huohuo, amewaonya wanaharakati dhidi ya kukiuka sheria kila wakati wanapojiandaa kufanya maandamano badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Image caption Wanafunzi waliofyatuliwa gesi ya kutoa machozi kwa kuandamana kupinga unyakuzi wa uwanja wao

Mnamo Jumatatu, wanafunzi watano na polisi mmoja walijeruhiwa katika vurugzu zilizotokea baada ya wanafunzi kuandamana kupinga unyakuzi wa ardhi yao kutoka kwa mtu aliyekuwa na mipango ya kufanya ujenzi.

Wakenya wamekosoa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanafunzi , hali ambayo imesababisha afisa ammoja mkuu kusimamishwa kazi kwa mda.

Shirika la kutetea masilahi ya watoto, la Save The Children, pia limelaani kitendo cha polisi dhidi ya wanafunzi hao ambao walikuwa wanaandamana kwa amani kutetea uwanja wao uliokuwa umenyakuliwa.