Chanjo dhidi ya Ebola kuwasili Liberia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chanjo dhidi ya Ebola kuwasili Liberia

Chanjo ya majaribio dhidi ya ugonjwa wa Ebola iko njiani kuelekea nchini Liberia.

Hii ni mara ya kwanza kwa chanjo hii kupelekwa kwenye nchi iliyoathiriwa zaidi na Ebola.

Lakini Wataalamu wanasema, wakati huu maambukizi ya Ebola yakiwa yanapungua,itakuwa vigumu kubaini kama chanjo hii inatoa kinga dhidi ya Virusi vya ugonjwa huo.

Chanjo hii ilitengenezwa na Kampuni moja ya Uingereza, GlaxoSmithKline (GSK )na Taasisi ya kitaifa ya afya nchini Marekani

GSK imesema ndege iliyo na dozi za awali takriban 300 za chanjo inatarajiwa kufika Monrovia siku ya ijumaa.

Kampuni ina matumaini mtu wa kwanza kujitolea atapata chanjo hiyo wiki chache zijazo.

Wanasayansi wanalenga kuwahusisha watu watakaojitolea takriban 30,000 katika majaribio hayo wakiwemo wafanyakazi wa afya.

Ikiwa taratibu zote zitafuatwa, Watu 10,000 watapatiwa chanjo ya GSK.

Haki miliki ya picha nihspl
Image caption Wataalamu wanaona itakuwa vigumu kubaini kama chanjo hiyo itafanya kazi

Idadi hiyohiyo ya watu watapata chanjo aina ya Placedo ,na wengine 10,000 chanjo nyingine ya majaribio.

Matokeo yatalinganishwa ili kubaini kama kuna chanjo yeyote kati ya hizo imefanya kazi dhidi ya Virusi vya Ebola.

Majaribio kama hayo tayari yalifanyika kwa wafanyakazi wa afya 200 waliojitolea nchini Uingereza, Marekani, Switerland na Mali.

Shirika la GSK limesema chanjo hizo zimeleta matokeo chanya.

Lakini ni kwa nchi zilizoathirika pekee ambapo wataalamu watasema kama inatoa kinga thabiti.

Kampuni inasisitiza kuwa Chanjo bado iko katika uboreshwaji na Shirika la Afya duniani, WHO na wakaguzi wengine wanakazi ya kuhakikisha kuwa wanajiridhisha kuhusu ubora na usalama wake kabla ya kampeni za matumizi ya kinga hiyo .

Chanjo hizo pia zimepangwa pia Guinea, Liberia,na Sierra Leone miezi kadhaa ijayo.