Hezbollah lashambulia jeshi la Israel

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wapiganaji wa Hezbollah

Kundi la wapiganaji wa Washia wa Lebanon walio chini ya vugu vugu la Hezbollah, linasema kuwa limetekeleza shambulio dhidi ya msafara wa wanajeshi wa Israeli katika mpaka wa mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake, Jeshi la Israeli linasema wanajeshi wake wanne wamejeruhiwa pale kombora lililorushwa kwa kifaru kupiga gari lake la kijeshi karibu na mpaka wa Lebanon.

Taarifa nyingine kutoka kwa Hezbollah zinasema kuwa zaidi ya waisraeli 15 yamkini wameuwawa au kujeruhiwa.

Kundi la Hezbollah linasema kuwa lilikuwa likijibu mashambulio ya angani yaliyofanywa na Israeli yaliyomuua jenerali mmoja wa Iran na wapiganaji kadhaa wa Hezbollah Nchini Syria siku kumi zilizopita.

Israel ilijibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora Kusini mwa Lebanon

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alionya kwamba jeshi la Israel liko tayari kutumia nguvu dhidi ya mashambulizi yoyote kutoka kwa washambuliaji.