Wanajeshi wa Chad waingia Nigeria

Image caption Kikosi cha kijeshi cha Nigeria

Vikosi vya Chad vimeingia nchini Nigeria kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Wanamgambo wa kiislamu, Boko Haram.

Msemaji wa idara ya usalama nchini Nigeria Mike Omeri amesema mapigano yalilenga eneo la kaskazini mashariki mwa mji wa Gamboru.

Kuingia kwa jeshi la Chad kunaelezwa kuwa sababu mgogoro na Boko Haram umefikia hatua ya kutoka nje ya mipaka ya Nigeria na kuathiri ukanda mzima.

Juma lililopita, Vikosi vya Chad viliripotiwa kuingia mjini Malumfatori, mji ulio karibu na mpaka kati ya Chad na Niger, baada ya mapambano dhidi ya Wanamgambo.

Kiongozi wa kundi la Boko Haram, Aboubakar Shekau ametishia kuanzisha matawi ya wanamgambo katika maeneo mengine nchini Nigeria,Niger,Chad na Cameroon.

Umoja wa Afrika una mpango wa kuunda kikosi cha Wanajeshi 7,500 kupambana na Boko Haram.