Busu katika kipindi lazua mjadala Angola

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu wa jinsia moja wapigana busu

Waandaaji wa kipindi maarufu cha tamthilia nchini Angola wameomba radhi baada ya sehemu ya Tamthilia hiyo iliyoonyesha wapenzi wa jinsia moja wakibusu kuamsha ghadhabu miongoni mwa watazamaji.

Televisheni ya Taifa imesema imesitisha Matangazo ya Tamthilia ya Jikulumessu kwa sababu za kiufundi.

Watazamaji wengi wanaona kuwa kipindi hicho kilivuka mipaka kwa kuonyesha wanaume wakibusu, ingawa haijatangazwa kuwa mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja nchini Angola ni haramu.

Kipindi hicho kilikuwa kinatengenezwa na Kampuni moja inayomilikiwa na Mtoto wa Rais.

Jose Eduardo Paulino dos Santos,Msanii maarufu nchini humo amekuwa akishutumiwa kunadi vitendo vya mahusiano ya jinsia moja miongoni mwa Jamii ambayo imekuwa katika misingi ya kuheshimu maadili na dini.

Kampuni yake,imesema inapitia tena vipindi vyake na imeomba radhi kwa kuwakera Watazamaji.

Kipindi cha Jikulumessu huangazia maswala yanayogusa jamii kama vile ndoa za mitara, mahusiano ya jinsia moja, biashara ya ngono kwa ajili ya kuzua mjadala kwenye jamii.