Mkakati wasukwa kumaliza mzozo Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption hali ya usalama nchini Ukraine imeendelea kuzorota kutokana na mapigano kati ya majeshi ya Serikali na Waasi wanaoiunga mkono Urusi.

Wakati mapigano yakiendelea mashariki mwa Ukraine, viongozi wa nchi za magharibi wamependekeza mipango mipya kujaribu kumaliza mgogoro kati ya Majeshi ya Serikali na waasi wanaoungwa mkono na Urusi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema mapendekezo mapya yaliyotolewa na kiongozi wa Ujerumani Kansela Angela Merkel, na rais wa Ufaransa Bwana Francois Hollande, yameongeza matumaini ya kumaliza mapigano.

Mpango huo utawasilishwa kwa Urusi Ijumaa, ambako Urusi imeahidi mazungumzo yenye manufaa. Lakini hatua ya Urusi kuwaunga mkono waasi wa Ukraine imeshutumiwa na Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, ambaye anazuru Ukraine ameitaka Urusi kuwaondoa wapiganaji wake na zana za kivita kutoka Ukraine na kuiruhusu Ukraine kulinda mipaka yake.

Seneta wa chama cha Republican kutoka jimbo la Ohio, Rob Portman, amesema Ukraine inataka msaada zaidi kutoka nchi za magharibi ili kujilinda dhidi ya mashambulio ya waasi:"Nilikuwa Ukraine wakati wa uchaguzi wa rais. Niliona ukweli kwamba Ukraine ilikuwa inaelekeza mtizamo wake katika nchi za magharibi. Wanaiona Marekani kama mshirika na kweli tunawaangusha. Wanataka uwezo wa kujilinda wenyewe.Nafikiri kilichotokea tangu wakati ule kwa miezi mingi iliyopita, hali imezidi kuzorota. Imekuwa ya vurugu zaidi, kuna askari wengi zaidi na raia waliouawa,Warusi wanazidisha hali kuwa mbaya, majeshi ya Urusi yako nchini Ukraine kwa mujibu wa taarifa zote tunazopata, na zaidi ya hapo wanazidi kutoa misaada zaidi kwa makundi yanayotaka kujitenga kutoka Ukraine. Na sisi kwa kiwango cha chini, na ninaposema sisi, sina maana ya Marekani, ni nchi za NATO na washirika wengine duniani wanatakiwa kuiwezesha Ukraine kujilinda". Amesema Seneta Portman.