Wapinzani walalamikia uchaguzi Nigeria

Haki miliki ya picha apc
Image caption Muhammadu Buhari

Upinzani nchini Nigeria umekosoa hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi hadi mwishoni mwa Mwezi March.

Chama kikuu cha upinzani cha APC kimesema hatua hiyo ni kikwazo kikubwa kwa Demokrasia nchini humo.

Chama hicho kimedai kuwa Jeshi la Nigeria limelazimisha kuahirishwa kwa Uchaguzi ili liweze kumsaidia Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan kwenye Kampeni zake.

Uchaguzi mkuu nchini humo ulipangwa kufanyika jumamosi ijayo lakini Tume ya Uchaguzi imesema Mashambulizi ya Boko Haram kwa kiasi kikubwa yanahatarisha uwepo wa zoezi la uchaguzi ,Usalama wa Wapigakura, na waangalizi wa Uchaguzi.

Hajiya Amina Zakari ni Afisa wa juu wa tume ya uchaguzi , INEC ameiambia BBC kuwa hawajashurutishwa isipokuwa walishauriwa kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi.

Kwa upande wake Seneta wa Lawali Shuaibu kutoka chama cha upinzani cha APC ameiambia BBC kuwa tishio la Boko Haram sio sababu ya msingi ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo.