Wahamiaji 200 wafa bahari ya Mediterani

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wahamiaji wakiokolewa bahari ya Mediterani baada ya boti walizokuwa wakisafiria kuzama.

Zaidi ya wahamiaji 200 wamekufa baada ya boti walizokuwa wakisafiria kuzama katika bahari ya Mediterani.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema"watu nane wameokolewa baada ya kukaa majini kwa siku nne. Watu wengine 203 wamezama baharini," msemaji wa UNHCR nchini Italia, Bi, Carlotta Sami, amesema hayo kupitia mtandao wa Twitter.

Ameitaja hali hiyo kuwa "msiba mbaya na wa kutisha".

Jumatatu wahamiaji wapatao 29 walikufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka kutokana na mawimbi makubwa.

Saba walikuwa tayari wamekufa wakati walipochukuliwa kutoka eneo la karibu na kisiwa cha Lampedusa, nchini Italia.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji limesema boti zote mbili zilizohusika katika ajali hiyo zilitoka pwani ya Libya Jumamosi.

IOM imesema kila boti ilikuwa imebeba zaidi ya watu 100 wakati zilipopinduka, huenda ilikuwa Jumatatu.

Watu tisa walionusurika wote wanazungumza Kifaransa na wanaaminika kuwa wanatoka Afrika Magharibi.